Mtazamo wangu kuhusu vurugu za Mtwara
Moja ya picha ikionesha moto mjini Mtwara, jana.(chini ni picha ya muasisi wa Taifa letu Hayati mwl. Julius Kambarage Nyerere, mzalendo wa kweli.)
Chanzo cha vurugu:
Vurugu hizo zilitokana na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusisitiza kuwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kuja Dar es Salaam litajengwa, jambo lingine linalodaiwa kusababisha ghasia hizo ni hatua ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutokurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge hivyo kuwakosesha wananchi fursa ya kusikiliza bajeti hiyo.
Pia vurugu hizo zilichangiwa na vipeperushi vilivyosambazwa na watu wasiojulikana wakitaka watu kuacha kufanya shughuli zozote na kukaa nyumbani ili kufahamu hatima ya mradi wa usafirishaji wa gesi kutoka Msimbati hadi Dar es Salaam kwa njia ya bomba.
Athari zilizotokea:
Waandishi wa TBC walitishiwa uhai wa maisha na mali zao. Nyumba na gari la mwandishi, Kassimu Mikongoro, vikachomwa moto na kuteketea kabisa. Pia nyumba za Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi) ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia zilichomwa moto.
Katika Mtaa wa Majengo, kundi la vijana lilivamia Ofisi ya CCM Kata na Ofisi ya Serikali ya Kata na kuanza kuzibomoa. Pia nyumba ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mtwara-Mikindani, Ali Chinkawene ilirushiwa mawe.
Ofisi ya Mtendaji Mtaa wa Msikitini, Kata ya Reli na Ofisi ya CCM Chikongola nazo zimeteketezwa kwa moto. Wanafunzi wa Shule za Msingi Shangani na Majengo walirejeshwa nyumbani baada ya mabomu ya machozi kurindima kuanzia asubuhi hadi mchana.
Mashuhuda wanasema mtu mmoja anaaminika kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa huku askari wanne wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), nao pia wakipoteza maisha katika ajali wakitokea Nachingwea kwenda Mtwara ili kusaidia kutuliza vurugu hizo. Katika ajali hiyo, askari 20 walijeruhiwa, wengi wao vibaya na saba walinusurika.
Tangu asubuhi kama ilivyokuwa Mei, 17 mwaka huu, Mji wa Mtwara ulikuwa kimya na huduma nyingi za kijamii zilisimama ikiwamo usafiri wa pikipiki, daladala, mabasi maduka na masoko.
Milio ya risasi na mabomu kama vitani:
Milio ya risasi za moto na mabomu ya machozi vilisikika kila kona na hasa Mitaa ya Mdenga, Magomeni na Shengena Mjini Mtwara ambako hali ilikuwa mbaya kutokana na kuwapo kwa mapambano kati ya polisi na vijana.
Turejee mifano:Rwanda:
Wakoloni Wabelgiji, waliikatakata nchi ya Rwanda katika makundi mawili, kutokana na mfumo wao wa utawala ili kujinufaisha na madini yanayopatikana magharibi ya nchi hiyo. Mfumo huo uliwakandamiza kimakabila, kabila la Watusti wakakwezwa na Wahutu wakashushwa kubakia wafanyakazi hasa mashambani wakati Watusti walikuwa wafanyakzi maofisini. Watusi na Wahutu, ni makabila makubwa nchini Rwanda. Wabelgiji walipoondoka kurudi Ulaya, Wahutu, wakapata nafasi ya kujitetea. Njia waliyotumia kutafuta haki ikawa vita. Mwaka 1994, ikazuka vita mbaya kuwahi utokotokea hapa Afrika Mashariki. Watu zaidi ya milioni moja waliuawa katika vita hiyo.
Rwanda ya leo:
Kwa sasa nchi hiyo, iko katika ramani ya moja ya nchi zenye uchumi mzuri katika Afrika Mashariki, sharia ya kukomesha ubunafsi wa tabaka za ukabila, inasimamiwa vilivyo. Ni kosa la jinai, kutaja kabila la mhutu au mtusi kuonesha tofauti zao. Vitambulisho vya utaifa vimendikwa Mnyarwanda, na sio Mhutu, Mtutsi wala Mtwa.
Mtazamo na maoni yangu:
Napozitazama vurugu hizi, Napata mawazo ya mbali sana kuhusu matokeo ya vurugu! Najiuliza swali moja kuu, kwamba, matokeo ya vurugu nini? Kama chanzo ni gesi hii isisafirishwe kuja jijini Dar es salaam, je huo sio ubinafsi?
Bila shaka ubinafsi wa aina hii katika nchi yetu ukiachwa uendelee, utapoteza maana halisi ya umoja wa kitaifa. Nasema hivyo kwa kumaanisha kuwa, kila mkoa unaweza kudai mali asili inayopatikana katika mkoa wake, iwe ni mali ya mkoa husika, jambo ambalo haliwezekani kabisa katika nchi yenye umoja uliotokana na ujamaa.
Wanasisa na wanaojiita wanaharakati, wadhibitiwe na kuadhibiwa pale watakathibitika kuhusika kwa njia moja au nyingine.
Binafsi, nitaendelea kuwalalamikia pia wakoloni. Sasa wanajifanya wataalamu na watoa misaada. Hawa, ndio wanaoleta chokochoko hizi. Sisi tupigane kwa kuonana wabaya ili wanufaike wao. Imani yangu inanituma huko kwa kuwa nikirudi katika historia ya vita nyingi zinazotokea katika bara la Afrika na mashariki ya kati, wazungu hawa, wanakuwa mstari wa mbele kukimbilia kutoa misaada ya kibinadamu. Kutoa kwao misaada, sikatai, ila wanaingiza faida kubwa sana nyuma ya vita wanazozitengeneza wao.
Wanauza silaha, maana nchi hizi hazina uwezo kiviwanda kuzalisha silaha!
Wanapora rasilimali muhimu na kuondoka nazo makwao.
Vurugu hizi za Mtwara, zina mikono ya watu wenye pesa na tamaa ya kujinufaisha wenyewe na familia zao.
Chokochoko za uvunjifu wa amani ya nchi yetu, zimeanzia mbali hadi kufikia Mtwara. Udini unaosmabaa chini kwa chini pamoja na ukabila.
Kwa hili srikali ikae chini na wananchi wa Mtwara, kuwaelewesha upya faida watakazopata juu ya ugunduzi huu wa gesi na iwe wazi kwao.
Wananchi pia waiheshimu serikali na kuwapuuza wachochezi hawa wenye nia mbaya na amani ya nchi yetu.
Waandishi na vyombo vya habari, wawe mstari wa mbele kuripoti kwa uweledi wa kizalendo habari zote zinazohusu Mtwara na gesi. Zisiandikwe au kutangazwa habari zenye uchochezi au zeney kuleta sintofahamu yoyote.
No comments:
Post a Comment