"Nilimsaidia Kikwete uchaguzi wa 2010" Lipumba

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua suala zito akikihusisha chama chake na “kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita.
Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa.
Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.
Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe, kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.
“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.
Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.
Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.

“Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe.
“Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.
“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh. Nilipokutana naye, alinipongeza; sijui kama yeye anakumbuka, akaniambia ‘umeweka mbele imani yako na umekuwa mwelewa wa mambo.’”
Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba kuwaambia Waislamu wajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hakusema wajipange kupitia chama kipi.
Lakini alisisitiza kwamba uchaguzi ujao ni zaidi ya siasa au rais yupi anafaa, bali maslahi, hasa ya rasilimali nyeti zinazopatikana katika ukanda wa Pwani ya Mashariki, eneo ambalo alisema linakaliwa zaidi na watu wenye imani ya Kiislamu.
Katika moja ya kauli zake, Profesa Lipumba alisema kwamba kuna chama kimoja kinataka kuchukua madaraka ya nchi, lakini kinasaidiwa na mataifa ya magharibi, yasiyoenzi wala kuthamini imani ya Kiislamu.

Kwa muda sasa, zimekuwapo tetesi kwamba CCM imekuwa inafanya siasa za udini dhidi ya vyama vya upinzani, hasa inapoona maslahi yake yapo hatarini.
Mwaka 2010 makada kadhaa wa CCM walitumia mitandao ya simu kuchonga (spoofing) ujumbe wa simu ulioshambulia mgombea mmoja wa upinzani, ukimhusisha na imani yake.
Kauli ya Lipumba imethibitisha pia minong’ono iliyokuwapo muda mrefu kuwa baadhi ya kura za Profesa Lipumba zilipotelea kwa Rais Kikwete.
Katika uchaguzi huo, Lipumba alitangazwa kushika namba ya tatu, nyuma ya Rais Kikwete na Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA.
Alipoulizwa kuhusu ziara yake msikitini na kauli aliyotoa, Profesa Lipumba alikiri kwamba alikwenda kuzungumzia hali ya kisiasa nchini.

2 comments:

Anonymous said...

Lipumba anapalilia udimi!hafai kuwa raisi wa nchi hii!

Anonymous said...

damu ya wananchi itayomwagika kutokana na machafuko ya mapigano ya kidini,Lipumba ahusishwe maana anaonekana wazi ndio kinara wa kuchafua amani