HATIMAYE KASYOME,AWA WA MTAANI!

Kutokana na mishemishe za kusaka mkwanja na life bora kwa kila mtz,nimeamua kuzidi kuchanja mbuga zaidi ili kufikisha ujumbe wangu kwingi zaid!
Kwa kuanzia naanza na kuzungumza hovo hovo kupitia magazeti!
Ukitaka kuamini usikose kufuatilia makala zangu kupitia gazeti la HOJA kila Alhamisiinayokimbilia kwa Mungu!Sikiliza moja ya makala utakazokumbana nazo pale:
Ni mwaka mwingine tena. Mwezi mwingine tena. Wiki nyingine tena. Siku nyingine tena na saa nyingine tena, ninapozungumza na watanzania wenzangu juu ya maisha na mafanikio. Kila mafanikio yana connection.
Namshukuru Mungu wangu wa mbinguni ambaye ni mwema kwangu kwa kuwa anaendelea kunisimamia na kunitangulia. Asante ee Baba.
Baada ya utangulizi huo ni vyema nikaanza na utambulisho wa makala zangu ambazo kwa majaaliwa ya mwenyezi Mungu, nitakuwa nikizitoa kila wiki, labda itokee vinginevyo.
Hapa tutakuwa tunazungumza na kujadili kuhusu ujana, elimu na burudani.
Mada ya elimu ndio itakayotangulia. Ufafanuzi sahihi wa elimu, ni mpana sana. Kwa ufupi tu niseme ,elimu ni mafanikio na maendeleo. Ukiwa na elimu ni vigumu sana kufa masikini.
Naomba nieleweke hapa. Napozungumza “vigumu kufa masikini,” namaamisha kuwa mbunifu katika maisha, kutegemewa kwa kuwa daraja la mafanikio kati ya, kugundua na kutumia mbinu mpya za mafanikio zinazokuwezesha kuishi wewe na familia yako au jamii inayokuzunguka n.k. Kwa ujumla, ukiwa na elimu, unakuwa mjanja zaidi na elimu inakupa urahisi wa maisha. Trust me. Yupo mwanasaikolojia mmoja kutoka nchi za ughaibuni aliyewahi kusema “no education, no life.” Hakumaanisha kwamba, bila elimu unakufa na kuzikwa. Hapana. Alichozungumza ni kwamba bila elimu huwezi kuwa na uhakika wa kufika kokote unakotaka kuelekea na kuyafikia mafanikio yako.
Japo wapo waliokosa elimu na ukiwatazama wana mafanikio makubwa sana, pengine kuliko wale wenye elimu, tena kubwa. Mara nyingi watu wa aina hii hupata pesa au mafanikio kwa njia haramu, kusota sana au wakati mwingine kurithishwa na ndugu au wazazi wao. Njia rahisi na nafuu ya kupata mafanikio ni kusoma tu; tena kusoma kwa malengo.
Ngoja nikupe mifano hai. Jjirani yangu, ni mtu mzima. Ana mke na watoto wawili; wa kike na wa kiume. Wa kiume ana miaka kumi na tano na wa kike ana miaka kumi na saba ambaye tutamwongelea leo. Mtoto huyu ameshamaliza kidato cha nne na anatazamiwa kuanza kidato cha tano mwaka huu kwa mfumo wa elimu ya Kitanzania.
Jana jioni alikuwa nyuma ya nyumba yangu akichana maneno katikati ya wavulana wawili walioonekana kumzidi miaka kama mitano au sita hivi mbele. Yeye alikuwa amekaa chini,huku wale vijana wamesimama pembeni yake wakiwa na vitabu mikononi. Kila dakika na sekunde zilipoyoyoma, nilizdi kuvutiwa na mazungumzo yao ya wale wavulana. Binti aliwang’ang’ania wamwelekeze kwa mshikaji wake aliyehama mtaa bila kumtaarifu. Alizidi kuwachafulia hewa kwa kudai kuwa anampenda mchizi na kwamba yuko tayari kuacha kuendelea na shule ili akaishi naye na kwamba elimu aliyoipata inamtosha. Duh. Bahati mbaya, muda huo umeme ukakatika. Nikashangaa kuona nyumba ya jirani kuna umeme na kwangu tu ndipo penye giza. Nikatahamaki na kuanza kuwayawaya mle ndani.Kumbe lahaulah, luku iliisha.
Haraka haraka nikatoka nje kwenda kununua na niliporudi binti na wale vijana sikuwakuta.Hivyo nilikosa mwendelezo wa story tamu. Sikukubali. Kama kawaida yangu ya udaku na upekuzi, asubuhi ya leo nikamdaka mmoja wa wale vijana ambaye nilimfahamu. Nikajaribu kumdadisi kuhusu kikao chao cha jana jioni. Akanitemea cheche zote.

Mungu wangu! Nililogundua ya kwamba binti alipigwa chini, aliachwa, na mchizi wake kwa kuwa alionekana hana future ya elimu.Mchizi ni mwanafunzi wa mwaka wa pili chuo kikuu na ni mjasiliamali pia.
Hapo hapo nikakuna kichwa na kuamini kuwa elimu ni kila kitu hasa kwa anayefahamu umuhimu wake. Lakini, nikajiuliza, “Ni nani anayestahili kumfahamisha na kumwelewesha umuhimu wa elimu mtu kama huyo?” Nikagundua ni yeyote mwenye nafasi na moyo wa kusaidia.
Ebu ngoja niishie hapa kwa leo ,maana jirani yangu hakunipa ruhusa ya kumwandika gazetini, ila kisa cha binti yake kimenikumbusha tatizo letu moja sisi vijana juu ya malengo ya elimu ya leo, ambayo ndio msingi wa maisha ya kesho.
Katika kila mwisho wa makala nitakuwa nikitoa anuani za vyuo ili kuwaunganisha wanaopenda kwenda kusoma nje ya nchi.

No comments: