RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.
Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.
Profesa Rwakabamba alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.
Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo.
No comments:
Post a Comment